Ukweli Kuhusu MATUMIZI YAKO ya Fedha

Matumizi ya fedha yanaonyesha wewe ni mtu wa aina gani

Je, umezoea kuhudumia watu?

Au ni mwekezaji na unathamini akiba,

Unapenda starehe, sherehe, urembo, mapambo, vifaa vya kielekroniki…

Mkeka wako wa matumizi, utakusaidia kupata majibu.

Ripoti ya Hali ya Upatikanaji na Matumizi ya Huduma za Kifedha nchini, FinScope Tanzania ya 2023, imeonyesha kwamba…

matumizi (ukitoa chakula na mavazi) ni kipaumbele cha matumizi binafsi kwa asilimia 77%,

huku jambo kama akiba ni kipaumbele kwa asilimia 4% tu.

Matumizi yako yanaonyesha:

1. Vipaumbele Vyako

Matumizi yako ya awali na makubwa yatakuonyesha vitu gani ni muhimu kwako;

kula vizuri, kulipa madeni, kununua nguo, kuhudumia familia, kufurahisha marafiki,…

kutoka ‘out’, kuweka akiba ya matumizi ya msingi, kuendeleza biashara nk.

2. Nguvu Yako ya Kuweka Akiba na Kuwekeza

Ni asilimia ya mapato yako inaenda kwa ajili ya maisha yako ya baadae,

✔ Akiba ya Dharura

✔ Mfuko wa Kustaafu (hauhusiani na NSSF, PSSSF)

✔ Kujenga Nyumba

✔ Kuwekeza Kwenye Rasilimali Fedha kama Hisa, Bondi, nk.

Inawezekana matumizi yako yanaonyesha huweka akiba kabisa, unaweka akiba kidogo,…

au kipato chako kinapoongezeka, kipi kati ya matumizi na akiba kinaongezeka.

3. Kama Kipato Chako ni Pungufu, Kinatosha, au Haukimudu Vizuri

Kama kipato chako cha mwezi kinatumika kwa matumizi ya msingi tu na hakuna ziada, basi kipato ni pungufu kulingana na uhalisia wa maisha,

lakini pia inawezekana kipato chako kinatosha lakini hakikupi nafasi ya kutimiza malengo yako yote ya kifedha,…

au una kipato kikubwa lakini haukimudu vizuri.

Tathmini kipato chako kulingana na matumizi ya msingi, akiba, na malengo yako ya kifedha kujua kama ni vipi itakubidi kuongeza,

ili uishi maisha unayoyataka.

4. Nidhamu Yako ya Pesa

Je, unajali kuhusu akiba?

Unaweza ukajiambia hapana kama matumizi yanayokuja hayaendani na malengo yako?

Unaweza ukasema hapana kwa wale waliozoea kukuomba hela na unajua hawatarudisha?

Je, pesa yako unaielekeza kuendeleza biashara, uwekezaji, na malengo yako ya kifedha kama ulivyokusudia?

Uwezo wako wa kusema ndio au hapana ndipo nidhamu yako ilipo.

5. Maamuzi Gani Yanaharibu Bajeti Yako

Inaweza ikawa,

✔ Matumizi ya Dharura

✔ Mlolongo wa Madeni, au

✔ Kuhudumia familia na marafiki

Ukijua matumizi yako kwa angalau mwezi mmoja, utapata majibu yako kwa urahisi.

6. Ni Makosa Gani ya Kifedha Ambayo ni Tabia Kwako

Kama tulivyosema awali kwamba,

Matumizi yanatokana na tabia. Kama unaweka nia na mipango haitimiii, ni tabia gani inabidi kubadilisha kwa upande wako?

Mfano, kama yafuatayo ni kawaida;

✔ Matumizi ya Dharura ~ inabidi kujenga tabia ya kutanguliza akiba

✔ Mlolongo wa Madeni ~ kuachana na tabia ya kukopa

✔ Kuhudumia Familia na Marafiki ~ kufanya kwa kiasi na kusema hapana

Haijawahi kuwa rahisi kubadilisha tabia, hasa ya kwako mwenyewe. Hivyo kuwa na subira na tafuta mtu wa kukuwajibisha.

7. Hali Gani Zinakusukuma Kufanya Matumizi Ambayo Haukuyapanga

Inawezekana sio tabia, ni hali za mara moja moja.

Kama ni,

huzuni (utanunua unachokipenda upate furaha kwa huo muda mfupi),

furaha (utatumia hela kuongeza zaidi hali uliyonayo),

hasira (utanunua unachokipenda ushushe hio hasira kwa huo muda mfupi), au

aibu (hautaki kuaibika kwa mpenzi, marafiki au familia: hata kama huna).

Katika hali ya huzuni, hasira, na aibu, hela inatumika kama kipozeo cha unachokihisi ila haitatui sababu ya hali hiyo kuwepo.

Unaweza kufuatilia matumizi yako ya mwezi kupitia kwa kupakua (download) tracker, kama inavyoonekana hapa chini;

au ukatumia apps za simu kama Moneylover, ambazo ni bure na rahisi kutumia, online na offline.

Na pia, unaweza ukajifanyia tathmini ya uchumi binafsi kwa kujibu maswali machache, kama inavyoonekana hapa chini;

Utatumiwa majibu yako kwenye email ili ugundue wapi pa kuanza kuboresha.

Usiache kufuatilia ukurasa wa Instagram kupata free content, na unaweza ukatuandikia kupitia Whatsapp.

PS:

Ndani ya dakika 60, jengo lililojengwa kwa miaka mitatu (3) linaweza kuteketea kabisa kwa moto,

Na ndio ilivyo rahisi kuimaliza pesa uliotumia nguvu kuipata na kuikusanya kwa muda mrefu.

Kujua na kuzingatia namna unavyotumia pesa ni muhimu!

Kwako wewe na kwangu pia.

Kila la kheri.

Wako katika pesa,

Gracing Money!

Marejeo:

1] FinScope Tanzania 2023

Share your love
Grace Sambali
Grace Sambali
Articles: 55